+255 753 204 743 mkumbosj@gmail.com, facebook.com/mwlsamwelmkumbo

Thursday, September 4, 2014

USALAMA NA UBORA WA NAFSI YAKO UNAVYOHUSIANA NA UHAI WA KANISA-2



TAZAMA NAMI:
Ni vema kuwa na furaha wakati wote, moyo wako uwe unaachilia kicheko, moyo wako uwe unabubujika furaha wakati wote, jiwekee hazina ya kicheko cha nafsi, jiwekee furaha inayoujaliza moyo wako wakati wote, nafsi yako isiwe na kuinama, itie nafsi yako nguvu nyingi wakati wowote.
Na:
Mwl. Samwel Mkumbo



Kuondoa ufahamu ulionao na kukuwekea
ufahamu mpya juu ya jambo Fulani
Sasa ufahamu mpya unapokuja ndani yako lengo lake linguine ni kutaka kuondoa ufahamu uliokuwa nao kwanza na kukuwekea ufahamu mpya kabisa aidha ni sahihi au si sahihi.
Mwanzo 3:4-5 tunasoma hivi;
Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.
Lakini katika mstari huo pia kuna kitu natamani nikuoneshe ambacho ni cha msingi sana sana, nacho ni jinsi shetani anavyoleta ufahamu wake, ufahamu wa shetani unakuja kwa mtazamo ya kwamba kuna Ukweli mwingi na Uongo kidogo, usidhani ya kwamba shetani kwa kuwa ni baba wa uongo basi atakuja kukuambia uongo kwa asilimia zote, la hasha! Lakini anakuja kwa mtindo ambao utaona kuna ukweli mwingi sana.
Angalia vizuri majibu yake kwa Hawa baada ya kujua Hawa anafahamu nini juu ya hilo alikuja na sentensi nyingi za Ukweli lakini maneno mawili tu ya Uongo, na anachokifanya shetani hawezi kuweka msisitizo kwenye yale mengi ambayo huwa ni ukweli, bali anaweka msisitizo kwenye lile moja au yale machache yaliyo ya uongo.
Angalia huo mstari tena;
Nyoka akamwambia mwanamke, HAKIKA hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.
Unaweza kuona ya kwamba pale penye maneno HAKIKA hamtakufa, ndipo penye uongo lakini ndipo shetani alipawekea Msisitizo, maana aliweka neno HAKIKA.
Huku kwingine hakuweka msisitizo wala hakuweka neno HAKIKA AU KWELI kwa sababu alijua ndio ukweli, sasa alichoweza kufanya ni kuweka msisitizo kwenye lile alilokusudia ambalo ni la uongo.
Mathayo 2:8 tunasoma maneno haya;


Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie.
Hebu tazama kwa makini maneno aliyoyasema Herode mwanzoni mwa maagizo yake ….mkaulize sana mambo ya mtoto;….. halafu angalia alivyomalizia sentensi aliyomalizia nayo .,. ili mimi nami niende nimsujudie……
Sasa msingi wetu tuliuweka katika kuangalia uhusiano wa nafsi yako au nafsi ya mtu mmoja mmoja inapokuwa salama na inapokuwa Bora inahusianaje na Uhai wa Kanisa.
MATENDO 20:28 inasema hivi;
Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. 
Na ukiutazama huo mstari kwa haraka unatupeleka kwenye hali ya kuamini kwamba Paulo alikuwa akisema na Viongozi, na ndivyo inatuonesha mistari inayotangulia mstari huo, hasa mistari miwili yaani wa 17-18.
Lakini nataka niweke jambo moja ndani yako ya kwamba ile tu mistari hiyo kuwekwa kwenye maandiko basi kwa namna moja inatuhusu na sisi, sasa nataka nikutazamishe jambo moja la msingi kidogo kutoka kwenye mstari ule wa 28. Hebu tuusome tena mstari huo;
Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. MATENDO 20:28.
Sasa hebu tuanzie na maneno yale Jitunzeni nafsi zenu,….. yaani Jihifadhini, Jilindeni, Jiwekeni Salama nafsi zenu,….halafu weka maneno haya ,…mpate kulilisha kanisa lake Mungu,…
Lakini maneno yaliyonipa Nguvu kuweka mstari huu kama msingi na kuutazama si kama mstari unaowahusu wazee wa kanisa, au wachungaji tu, au maaskofu tu, au wahubiri au watu wenye vyeo vya aina Fulani katika kanisa ni yale maneno yanayosema hivi; …ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake….
Ni ngumu kuelewa kwanini neno hili WAANGALIZI lina umuhimu sana katika mstari huu, na ndilo linalotufanya tujifunze umuhimu wa kuzitunza nafsi zetu kwa ajili ya uhai wa kanisa, neno Mwangalizi wakati mwingine linatumika kama Askofu, yaani mwangalizi.
TAZAMA NAMI:
Neno askofu kwa utaratibu wa cheo ni MCHUNGAJI WA WACHUNGAJI, lakini kwa utaratibu wa Wokovu na Kiroho ni mtu yeyote ambaye Nafsi yake AMEIUNGANISHA na Kanisa ya kwamba yupo kuhakikisha kila jambo linalotakiwa kwenye kanisa linaenda kama itakiwavyo, aidha kwa maombi yake au kwa mali zake.
Tito 1:7 tunasoma maneno haya;
Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno ,kwa kuwa ni wakili wa MUNGU; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake,asiwe mwepesi wa hasira,asiwe mlevi wala mgomvi,asiwe mpenda mapato ya aibu.
Sasa kutoka kwenye mstari huo nataka tuweke mambo kadhaa ambayo ni ya msingi sana kuyaelewa ambayo ukiyaangalia kwa jicho la ndani utagundua ya kwamba ASKOFU ni mtu wa aina gani, na maneno yenyewe ni yale yanayotoa sifa za Askofu…
….asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu.
Ukitazama hizo sifa za Askofu utagundua ndizo sifa anazotakiwa kuwa nazo kila mtu aliye ndani ya kanisa, sasa basi hebu tuunganishe na somo letu uone maana itakayotokea, maana yake kama tunajua nafsi ya kila mmoja ina umuhimu katika kanisa na ya kwamba kila nafsi ikiwa Salama na ikiwa Bora basi kuna uhakika wa Kanisa kusimama Imara na kuwa na Uhai wake.
Waebrania 12:15 tunasoma;
Mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.
Uchungu ukiingia nafsini mwa mtu anayeamini unazaa manung’uniko, na manung’uniko yakiwepo basi kazi ya Mungu au kama ni kanisa basi haliwezi kuendelea mbele hata kidogo, haijalishi hayo manung’uniko hayatoki kwa viongozi au yanazalishwa na mtu asiye na nafasi kubwa kwenye kanisa lakini manung’uniko ni matokeo ya jeraha ya nafsi.
TAZAMA NAMI:
Manung’uniko au maumivu yanayotoka kwa watu walio ndani ya kanisa au watu wanaoliongoza Kanisa au hata Familia yana sumu mbaya sana kuliko kitu chochote maana yanaleta hali ambayo mioyo ya watu inakosa kicheko, na hakuna kitu kibaya moyo ukikosa kicheko, moyo ukikosa furaha, unaweza ukawa unakula lakini hauna afya nzuri kwa sababu ndani ya moyo hakuna kicheko, unaweza ukawa unacheka mdomoni lakini moyoni hakuna kicheko hivyo umebeba majeraha ya uchungu ndani yako.
Ogopa fellowship ambayo watu wana uchungu, nafsi zao zimeharibika, hata kama ni watoto walio ndani ya kanisa, au hata kama ni mtu asiye na sifa kubwa ndani ya familia yako lakini angalia nafsi yake isije kubeba uchungu,
Ni vema kuwa na furaha wakati wote, moyo wako uwe unaachilia kicheko, moyo wako uwe unabubujika furaha wakati wote, jiwekee hazina ya kicheko cha nafsi, jiwekee furaha inayoujaliza moyo wako wakati wote, nafsi yako isiwe na kuinama, itie nafsi yako nguvu nyingi wakati wowote.
Jisemee moyoni mwako hata kama hatuli vizuri nyumbani hata kama hatukai kwenye sofa hata kama kanisani kwetu hakuna vyombo vya mziki, hata kama watoto wangu hawana nguo mpya katika msimu huu wa sikukuu, hata kama ninaona wenzangu wanabadilisha magari au wanabadilisha nguo kila ibada au hata kama wapo watu wasiookoka wana fedha kuliko nilivyo mimi au wana nyumba nzuri kuliko ya kwangu lakini bado nafsi yangu itakuwa na furaha maana nimepata cha thamani kuliko vyote nimepata mmiliki wa vyote,,, YESU KRISTO, MUNGU WA KWELI, YEYE ALIYE UZIMA,,, Naaam nitajilinda NAFSI YANGU maana ninajua uzima wa mtu haupo katika wingi wa vitu alivyonavyo.

Luka 12:15 inasema hivi;
Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.

Itaendelea…  DOWNLOAD HERE

No comments:

Post a Comment

Home