Tunapoliendea jambo hili, kuhusu Torati inapobadilika na kuwa Neema, ni vizuri tukianzia hapo kwenye mkanganyiko kwa swali la msingi:
Je, kuna Andiko lolote linalotuambia na kutuamuru kuadhimisha Jumapili kama tu Wayahudi walivyoadhimisha Jumamosi?
Jibu ni hakuna. Hakuna Andiko lolote katika Biblia, haswa Agano Jipya, kwetu sisi Kanisa, linalotuamuru kuadhimisha Jumamosi wala Jumapili. Lakini kusudi la kuadhimisha Jumapili, ni ukumbusho wa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristo!
Sasa, kuna makundi yanasema, “Katoliki ya Kirumi ndio walioigeuza siku hiyo kutoka Jumamosi kuja Jumapili.” Nao Katoliki wanadai kulifanya jambo hilo, bali ni uongo mtupu. Kama ni wao walilifanya, basi mtakatifu Paulo atakuwa alikuwa ni Mkatoliki wa Kirumi, na hata Petro pia, Yohana, na Yakobo na wengineo wote, kwa kuwa wao walikutanika siku ya kwanza ya juma kwa ibada (Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, … Mdo 20:7). Na, kulingana na historia, njia pekee wangewatofautisha kati ya Wayahudi Wakristo na wale Wayahudi wa kiasili (orthodox), ilikuwa ni siku zao za ibada, orthodox walikutanika Jumamosi (waliokataa kufufuka kwa Kristo), na hawa wengine, Wakristo, wao walikutanika Jumapili (walioamini kuwa Yesu alifufuka katika wafu). Na hiyo ilikuwa ni alama ya utenganisho kwao. Na bado inaendelea kuwa ni alama, na huenda ikaja kuwa ile chapa ya ya mnyama!
Sasa, ndugu zetu Wasabato wao wanaamini kuwa kuitunza sabato, katika maana ya siku ya Jumamosi, huo ndio muhuri wa Mungu. Wao wanasema, “Unatiwa muhuri kwa kuadhimisha sabato.” Lakini hakuna Andiko hata moja katika Biblia lisemalo hayo. Yaani kimsingi tunaweza kusema kwa uhakika kuwa hilo ni fundisho lililo kinyume na Maandiko. Kwa faida gani? Roho aliyelibuni atakuwa anajua zaidi, ila halina uhusiano wowote ule na mbingu!
Lakini ukitaka kujua kuhusu muhuri wa Mungu, hebu lifananishe jambo hilo la muhuri wa Wasabato na Andiko hili katika Waefeso 4:30 “Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.” Ubatizo wa Roho Mtakatifu, Huu ndio muhuri wa Mungu! Unaona, ukienda katika Isaya 28 anasema, “Amri juu ya amri, kanuni juu ya kanuni, huku kidogo na huku kidogo.” Usikurupukie neno lolote bila kupata uhakika wa Maandiko katika Hekima yake!
Tazama, watu wanajaribu kufanya jambo fulani ili kujiokoa, wengine wanaacha kufanya kazi, wanajaribu kuacha kula nyama, wanajaribu kuadhimisha siku ya sabato ya Kiyahudi, wanajaribu hiki na kile, unaona, lakini hakuna kitu unachoweza kufanya kuhusu kujiokoa. Hivyo ndivyo ilivyo tabia ya mwanadamu wa mwilini, “Kama ungalifaulu kuacha pombe, au uzinzi, au kuvuta sigara, au ukiitunza sabato…”, hakuna utakalo fanya liwezalo kukuokoa! Tunaokolewa kwa Neema. Mungu hutuita, Mungu hutuokoa. Tunapaswa kuzifuata nyayo za Mungu, Neno lake, hicho tu. Naye Mungu kwa neema hutupatia Uzima mpya, huo Uzima wa milele. Nao Uzima wa milele ni Ubatizo wa Roho Mtakatifu! Sasa iwapo umedanganywa kuwa kwa kuitunza kwako sabato ya Kiyahudi ndio umetiwa muhuri, itakuwaje? Unaiona hasara hiyo, au umedanganywa kuwa ulipoNena kwa Lugha ndipo ulitiwa muhuri, hakika kama hautayafuata Maandiko UTAPOTEA!!!
Basi, Sabato ni nini? Sabato maana yake ni “Raha” ndipo Sabato yapaswa kuwa ni siku ya “raha!” kwahiyo unapoliona neno sabato, jua maana yake ni ‘raha’. Basi kwa vile jambo hili la sabato limo katika zile Amri Kumi, ambazo kimsingi ndizo zinazoleta mkanganyiko katika madai ya kuzitimiza kwake, kulingana na zilivyotolewa na kukabidhiwa Israeli, naye Kristo kwa kauli yake akisema kuwa hakuja kuitangua Torati, nazo Amri hizo zikiwa ni sehemu yake, hilo likimaanisha kuvushwa kwake kutoka Agano la Kale kuja Jipya. Ndipo makundi ya kikristo, hao wanaokutanika siku ya Jumapili huonekana ni wenye kuivunja Amri hiyo ya Nne, ambapo sababu zake nilizielezea huko juu. Nako kuvunjwa kwa Amri yoyote kati ya hizo, huhesabika ni kuvunjwa kwa zote. Ndipo sasa, nataka tulitazame jambo hili katika ujumla wake wa hizo Amri Kumi, ili kuona kwamba, tunapozizungumzia hizo Amri Kumi baada ya kumpokea Kristo, je, huwa tunazizungumzia hizo Amri katika maana ya zile walizopewa Israeli au zilizotimilizwa?
Kwa kadiri ya ile alama ya utenganisho, kule kukukataa kufufuka kwa Yesu kutoka katika wafu, kwa upande mmoja, na huko kuamini kuwa Yesu alifufuka katika wafu, nayo alama ya utenganisho huo ikijiwakilisha katika siku za kukutanika, Jumamosi kwa wanaokataa na Jumapili kwa walioamini, ndipo hata Amri hizo zimegawanyika kulingana na utenganisho huo. Kundi la waliokukataa kufufuka kwake Yesu likiendelea katika zile Amri Kumi za Agano la Kale, na hili kundi jingine lililokupokea kufufuka kwake, likiendendelea katika Amri zilizobadilishwa, yaani zilizotimilizwa! Basi mara nyingi tatizo huwa hapa, sote hudhani tunaongelea jambo moja lakini ukweli ni kwamba sisi huongelea vitu viwili tofauti, only similar!
Haya, na tuyatazame mambo yalivyo katika Agano Jipya. Kristo, katika Mathayo mlango wa 5 anaweka msingi wa jambo hili, “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.” Sasa Andiko hili linatudhihirishia kuwa Torati aliyoikuta Kristo, hiyo iliyokuwepo, katika ujumla wake, toka ilipotolewa na kutumika katika kuyaongoza makundi ya Israeli, ilifaa katika kazi hiyo ya uongozi (schoolmaster), yaani ikiwafundisha kuhusu dhambi na adhabu zake hapo inapowapeleka kwa Kristo. Hiyo ndiyo safari ya kiroho ya Israeli, kutoka utumwani hadi kuwa wana katika Kristo! Kwahiyo twaweza kusema kwa uhakika kuwa Torati au zile Amri, zimedumu hadi Kristo alipozitimiliza. Kwahiyo kundi lolote ambalo linaendelea katika hizo Amri zisizotimilizwa, hilo linahesabika pamoja na hao waliokataa kufufuka kwake Kristo, haijalishi kelele zao, matunda yao ndiyo yanayothibitisha kile walicho, nayo miti huzaa kulingana na pando au mbegu!
Lakini kwa upande wa pili, hawa wako katika torati iliyotimilizwa. Twaweza kuona kutimilizwa kwake kwa kuviangalia vifungu vichache vya Maandiko ili kuibaini maana kamili ya KUTIMILIZWA kwa Torati, yaani AGANO JIPYA! Basi Kristo anaanza hivi:
Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, ““Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu.”” Ati, hii ilikuwa ni nini? Torati, zile Amri.
Bali mimi (Yesu) nawaambieni, ““Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto.”” Akaigeuza hiyo Torati, sivyo? Huko kutimilizwa!
Mmesikia kwamba imenenwa, ““Usizini””; lakini mimi nawaambia,Aliigeuza, sivyo? Wadhani yeye hakuigeuza Torati? Vema, yeye alisema“”Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.””
Haya hayakuwepo kule nyuma katika Agano la Kale, haya ni Agano Jipya! Yeye alivuka ng’ambo na kuendelea kutoa Amri hizo, “Mmesikia wakisema, wale watu wa kale, ‘Usi…’ nami nawaambieni vinginevyo. Mmesikia wakisema, ‘Jino kwa jino na jicho kwa jicho,’ lakini mimi nawaambia…!
Sasa mwishoni mwa hayo yote, Yeye aliiacha ile Amri ya Nne, hiyo ilihusu, “Ikumbuke siku ya sabato na kuitakasa.” Sasa tazama, “Kila aziniye hana budi kupigwa mawe,” iliwabidi wawe katika tendo la kuzini. Sivyo? Na ilibidi wakamatwe katika tendo hilo. “Kila auaye,” ilibidi awe muuaji, awe ameua kihalisi.
Lakini Yesu anasema, “Kila amtazamaye mwanamke,” nafsi yake, roho, hakuna lolote katika mwili wake sasa, Nafsi yake ikiwa imekombolewa sasa, bali huko nyuma katika Torati, haikuwa imekombolewa wakati huo, kwani Torati ilikuwa ni kiongozi katika kuwaleta na kuwafikisha katika huo ukombozi wa Nafsi zao. Ndipo Yeye sasa akasema, “Kila amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.” Akasema, Mmesikia wakisema ‘Usiue,’ bali nasema kila amuoneaye ndugu yake hasira, amekwisha ua.” Unaiona Torati inavyotoka mwilini na kuhamia rohoni?
Basi Yeye alisema, yaani kuhusu sabato:
“Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha… ; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”
Umeiona hiyo sabato au pumziko au raha inayoahidiwa kwa Nafsi zetu? Si kwa mwili huu unaoonekana, Nafsini mwako!
Haya hebu msikilize Paulo sasa, akiwaandikia Waebrania, watu wa Torati, waadhimisha sabato. Sasa, anawaleta Wayahudi, kwa vivuli na mifano, akionesha kile Torati ilikuwa kwa mfano. ”Torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuja,” naye aendelea mbele kuinyonyesha kama mwezi na jua. Kama mwezi ulivyo kivuli cha jua, jua likiangaza sehemu fulani ya nchi, nao mwezi ukipokea kutoka kwa jua na kuangazia sehemu nyingine mwanga hafifu nk unaweza kuyaona hayo katika Waebrania 9. Lakini katika Ebr 4, anaingilia jambo la sabato. Sasa tazama,
Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa.
Paulo akinena na watu wa sabato, hao walioiadhimisha sabato. “Basi na tuogope ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika siku ya sabato” kwa maneno mengine!
“Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao(nyuma kule chini ya Torati)… Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliosikia.”
Sasa, hayo ni kule nyuma chini ya Torati. Hawakuwa na Imani, sababu hakukuwa na msingi wa kuiwekea. Umeona? Torati haina uwezo wa kuleta Imani, “Imani huja kwa kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo”
“Maana sisi tulioamini tunaingia katika (sabato) raha ile; kama vile alivyosema, …”
Sasa, raha “Yake”. Sasa “Yake” ni Raha ya Kristo. Raha yake, “Sabato” Yake! Si mnakumbuka tulikubaliana kuwa neno Sabato maana yake ni ‘raha’; kwahiyo kila palipoandikwa ‘raha’ tutatumia neno sabato ili tuupate ufahamu kuhusu kuadhimisha siku fulani. Haya,
“Maana sisi tulioamini tunaingia katika (Sabato) raha ile; kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia (Sabato Yangu) rahani mwangu:… (Sasa, tazama ujumbe wa Paulo wa siku iliyotakaswa)… ijapokuwa zile kazi zilimalizika tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu. Kwa maana ameinena(katika Torati) siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote.”
Hiyo ilikuwa ni siku Yake ya saba. Sasa, Paulo anakubali kuwa Mungu aliwapa wao, hiyo ilikuwa siku ya saba. Na Mungu alistarehe siku ya saba, akaibariki siku ya sabato, akaitukuza, na akaitakasa, akifanya siku ya kustarehe. Mungu akafanya hivyo, akaacha kazi Zake zote.
Na hapa napo, Hawataingia (Sabato Yangu) rahani mwangu (Yesu akinena).
Sasa, kuna sabato nyingine mahali fulani, iko wapi?
Basi, kwa kuwa neno hili limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao, …
Aweka tena siku fulani, …
Aweka siku hapa. Ni ipi? Sabato, sivyo? Aweka siku ya saba ya juma hapa kama sabato katika mahali hapa.
Aweka tena siku fulani, akisema katika Daudi baada ya muda mwingi namna hii, Leo; (hata Yesu alipokuja, ule wakati wa kwanza) … kama ilivyonenwa tangu zamani (Torati), Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu. (Mimi na wewe! Hapa kuna raha / Sabato nyingine ijayo; si ya kimwili, ya kiroho!)
Sasa, tungeweza kusema kwamba tuna siku ya saba pia. Twende taratibu, tuzifuate hatua Zake atuongozaye. Hebu tusome kifungu kinachofuata, tuone zaidi kuhusu hilo:
“Maana kama Yesu angaliwapa (Sabato) raha, asingaliinena siku nyingine baadaye.
Kristo alipoigeuza Torati, kutoka hiyo Torati hadi kuwa Neema, si angaliwapa siku nyingine ya ‘raha’ au sabato, siku fulani ya raha, siku fulani? Lakini Yeye hakusema lolote kuhusu sabato. Hakusema lolote kuhusu Jumapili, hakusema lolote kuhusu Jumamosi. Bali alisema hivi, Paulo kasema. Haya fungua hayo macho yako ya rohoni, usome na Mungu akupe ufahamu wake:
Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu. (Hiyo ni leo!)
Kwa maana yeye (mimi au wewe) aliyeingia katika raha yake (Raha ya Yesu, au sabato ya Yesu; “Njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha”) amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi zake. (hapo mwanzo).
Amina! Ndiyo hiyo sabato yetu, Ubatizo wa Roho Mtakatifu!!!
Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi. (kwa kung’ang’ana na siku, na kwingineko)
Tazama, Mungu alistarehe siku ya saba, akaiumba siku ya saba, akawapa Wayahudi kwa ajili ya ukumbusho, ikiwa imefungwa ndani ya Torati. Naye Paulo akiwa ni Myahudi, basi twadhani kuwa yeye alikuwa akiizungumzia siku hiyo waliyopewa? Angehesabiwa Haki kwa lipi? Maana twafahamu kuwa kwa Torati usingeHesabiwa Haki, bali yeye anayafundisha haya yote kwa uongozi wa RM. Ndipo unamuona akiyatia muhuri wa RM mafundisho haya, sawa sawa na Neno la Kristo hapo aliposema, “…bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao”, naye mt Paulo anasema, “Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe.” Huo ndio udhahiri wa Injili!
Basi ukipenda kujua Raha ya Wakristo ni nini, nenda katika Isaya 28, isomeni sura yote. Yeye alisema, ““Amri juu ya amri, kanuni juu ya kanuni, huku kidogo na huku kidogo…” Shikilia sana yale yaliyo mema.
La, bali kwa midomo ya watu wageni, na kwa lugha nyingine atasema na watu hawa; ambao aliwaambia, Hii ndiyo raha yenu, mpeni raha yeye aliyechoka; huku ndiko kuburudika; lakini hawakutaka kusikia.
Hii ndiyo sabato, ile raha ambayo walipaswa waingie. Bali kwa haya yote walifanya mioyo yao migumu na kutikisa vichwa vyao kuikataa. (Jambo lile lile tu walilolifanya siku ya Pentekoste, RM aliposhuka juu ya watu Azusa, na RM alipotolewa kwa watu kwa mara ya kwanza nyuma kule katika siku ya Pentekoste. Hiyo ndiyo Raha, sabato kwa watu wa Mungu)
Kwahiyo, sababu pekee tuadhimishayo Jumapili, ilianzishwa na baba zetu wa imani, Biblia, mtakatifu Paulo, Yohana, Mathayo, Marko, Luka na wengine wote, walienda nyumba kwa nyumba, wakifanya ushirika siku ya kwanza ya juma, mitume walipokusanyika na iliitwa, si sabato, bali siku ya Bwana. Yohana alisema, kwenye kile kisiwa cha Patmo, “nalikuwa katika Roho siku ya Bwana.” Sasa siku ya Bwana ni hiyo aliyofufuka, na ndipo yeye Yohana aliyaona hayo!
Hata ukiwarudia wana historia, kama Josephus na wengineo wengi wa mashariki, au wanahistoria wa kanisa, na wengineo wengi tu, waweza kuliona jambo hilo la kundi hili la Wakristo kukutanika katika siku hiyo ya Bwana. Katika kuwatofautisha, mmoja wao aliwaita ‘cannibals’ yaani “wala watu,” hao walikuwa ni Wakristo. Wao walisema, “Kuna mtu aliyeuawa na Pontio Pilato na wanafunzi wake wakaja na kuiba mwili wake. Nao wakauficha, na kila Jumapili wao huenda kula sehemu yake.” Lakini wao walikuwa wakifanya ushirika tu, wao walikuwa wakila mwili Wake na kunywa damu Yake! Wao walisema walikuwa wakila mwili wa Bwana, ushirika. Nao hawakujua ilikuwa ni nini, ndipo wakasema, “Walikuwa wala watu”, wakisema, “Wao huenda kuula kwenye siku ya kwanza ya juma, wao hukutanika pamoja na kuula mwili wa mtu huyo”
Nayo njia pekee ambayo ungetambua kama walikuwa waadhimisha sabato na wakanushaji kabisa wa ufufuo, ama walikuwa ni Wakristo na waaminio ufufuo, wengine walienda kanisani Jumamosi na wengine walienda kanisani Jumapili, hiyo ndiyo ilkuwa ALAMA kati yao, huko nyuma, na ingali ALAMA leo hii!!!
No comments:
Post a Comment